Showing posts with label new year. Show all posts
Showing posts with label new year. Show all posts

Thursday, December 31, 2009

Happy New Year... Heri ya Mwaka mpya na kwaheri 2009

Today I would like to share this poem written in Swahili by a talented young man studying in Turkey. An Eulogy to 2009.

NAONDOKA!
>
>
> Shairi naliandika, Natumai mko poa
> Izraili amefika, Roho yangu kuitoa
> Mwito kifo naitika, Meshindwa kujiokoa
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
> Ni miezi na masiku, Nami nimevumilia
> Nakumbuka ile siku, Nilipo waingilia
> Tena mida ya usiku, Nyote mkasubiria
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Saa zenu kwa pamoja, MlifUata akrabu
> Kwa sekunde mojamoja,Mkaweza kuhesabu
> Nne tatu mbili moja, Mkanambia karibu
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Hoye mkafurahia, Kwa shangwe mkanilaki
> Tena mkashangilia, Mukawasha mafataki
> Kwa masoda na mabia, Hakuna kilichobaki
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Awali mlinipenda, Na wala hamukugomba
> Elfu mbili na kenda,Kwenu ni mgeni bomba
> Ili nisiweze kwenda, Kukicha mkaniomba
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Tumekuwa marafiki, Wa kufa na kuzikana
> Tulogawana riziki, Wala hatukunyimana
> Hasa wakati wa dhiki,Daima tulifaana
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Vipi leo mwachukia, Kunilani kwa matusi
> Tangu nilipoingia, Ni mafua na virusi
> Mwatamani nifukia, Mpate ondoa nuksi
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Serikali zalalama, Mgeni mie sifai
> Uchumi umeshazama, Benki zinawadai
> Bidhaa zote gharama, Mpaka mumenikinai
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Namaliza msafara, Nilikuwa tu mgeni
> Mliopata madhara, Mtapata afueni
> Mliokula hasara, Nasema tena poleni
> Hata hivyo yote tisa, Kumi mie naondoka
>
>
>
>
> Hivi sasa nawatoka, Bora tu niwaacheni
> Kuwa nanyi nimechoka,Kwaheri nawaageni
> Sina budi kuchomoka, Yupo mwengine mgeni
> Hata hivyo yote tisa, Kumi roho yanitoka
>
>
>
>
> Mpokeeni mwenzangu, Anayefanana nami
> Jina lake kama langu,Elfu mbili na kumi
> Tabia ni kama zangu, Msimpige mangumi
> Hata hivyo yote tisa, Kumi roho yanitoka
>
>
>
>
> Kiumri nimemzidi, Hawezi kutabirika
> Basi namujitahidi, Kabla yeye kufika
> Mabadiliko yabidi, Msije kuathirika
> Hata hivyo yote tisa, Kumi roho ishatoka
>
>
>
>
>
> HAMZA A. MOHAMMED a.k.a 2009
>