Tuesday, August 25, 2009

Ramadhan Kariim

I received this poem in Swahili and I would like to share it as it reflects on Ramadan. I wish everyone a Ramadhan Makbul.

YA RABBI UTUNUSURU

Ninaanza kwa salamu, Baraka nizifaidi
Nashika yangu kalamu,Kusema imenibidi
Enyi ndugu isilamu, Umati wa Muhamadi
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Mikono naifungua, Na kwa moyo mkunjufu
Mgeni ameshatua, Mwezi mwema mtukufu
Naupokea kwa dua, Na furaha sufu sufu
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Mwaka huu mtihani, Si rahisi ni mgumu
Kuifunga Ramadhani,Mchana kutwa saumu
Kwa kweli sio utani,Yapaswa kujilazimu
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Daku msilisahau, Mkatafuna vitende
Ugali au pilau, Msipokula ni mbinde
Mujipige angalau,Saumu isiwashinde
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Mchana jua ni kali, Lazima kuvumilia
Magharibi nayo mbali,Adhana kusubiria
Ukahisi huna hali, Na ari kukuishia
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Sio matumbo pekee, Nafsi pia fungani
Macho msikodolee, Maovu kuyatamani
Ubora ni mtembee, Mkitazama angani
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Tena nchi za ulaya, Mazingira ni hatari
Watu wamekosa haya, Kwa kupenda ufahari
Tabia zao ni mbaya, Kwao kufunga hiari
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Hiyo miji ya likizo, Msimu wa kiangazi
Ndio kuna matatizo, Wanawake wote wazi
Kuvaa sio kigezo, Vimini ndio mavazi
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Tumuombe Maulana, Ya Allah ya Karimu
Tusijeipata lana, Kwa mambo yaso muhimu
Tutendeni ya maana, Isitupate hukumu
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


Tamati nimefikia, Imepita alasiri
Magharibi meingia, Namalizia shairi
Wenzangu nawakimbia,Nenda tafuta futari
Ya Rabbi utunusuru, Pepo tusijeikosa


by Hamza A. Mohammed